Polisi Waanda Mpango Mkakati Wa Ulinzi Shirikishi
Mkuu wa Polisi wilaya
ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto akiongea na wakazi wa Mtaa
Kitalu "D" Njiro katika mkutano uliofanyika tarehe 18.11.2012 juu ya uanzishwaji
wa vikundi vya ulinzi shirikishi
Mwenyekiti wa Mtaa wa
Kitalu "D" Njiro Bw.John Kihwele akihesabu fedha zilizopatikana baada ya Mkuu wa
Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto (kushoto
kwake) kuchangisha fedha hizo kwa njia ya harambee katika mkutano
uliowajumuisha, askari Polisi, viongozi wa Mtaa na wakazi wa eneo hilo
uliofanyika tarehe 18.11.2012.Jumla ya fedha taslimu Tsh 125,000 zilipatikana
papo hapo.
Picha na Mahmoud AhmadArusha
Na: Rashid Nchimbi wa
Polisi Arusha
Wakazi
wa Njiro mtaa wa Kitalu “D” wametakiwa kutolifanyia mzaha suala la uanzishaji
wa vikundi vya ulinzi shirikishi kwa madai kuwa wanajitosheleza katika suala
hilo. Akiongea na wakazi hao Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi
wa Polisi Gilles Muroto alisema kwamba suala la ulinzi halihitaji ubinafsi wala
masihara bali linahitaji ushirikiano wa hali juu.
“Tatizo
nililoligundua hapa kila mmoja anaona ameshajitosheleza katika suala la ulinzi
kwa kuwa ana mlinzi, kamera na uzio wa umeme, wakati suala hilo linahitaji
ushirikiano mkubwa”. Alionya Muroto .
Aliwataka wakazi hao
wachukue hatua za haraka juu ya uanzishaji wa vikundi hivyo ili kutotoa mwanya
kwa wahalifu kwani udhaifu walionao unaweza kutoa mwanya kwa wahalifu kuvamia
eneo hilo.
Alimuagiza Mwenyekiti wa
mtaa huo kukaa na wakazi hao ili kupitisha maazimio juu ya uchangiaji wa vikundi
hivyo na mara baada ya kukubaliana sheria hiyo itakuwa ni miongoni mwa sheria za
serikali ya mitaa hivyo basi yeyote atakayekaidi atachukuliwa
hatua.
Aidha
aliwataka viongozi wa mtaa huo kuwafahamu watu wote wa eneo hilo hivyo kusaidia
kubaini tabia ya kila mmoja na pia kila mtu awe na mawasiliano ya simu na
mwezake jambo ambalo litasaidia kupeana taarifa pindi uhalifu
unapotokea.
Katika
kuhamasisha kufufua vikundi hivyo vya ulinzi shirikishi Mkuu huyo wa Polisi
Wilaya alianzisha harambee ya kuchangisha fedha kwa kila mkazi aliyehudhuria
mkutano huo hali ambayo ilisaidia kupatikana kwa fedha taslimu Tsh 125,000 papo
hapo huku yeye mwenyewe akiwa wa kwanza kutoa mchango
wake.
Aliongeza kwa kuwaambia
wananchi hao katika kuimarisha vikundi hivyo, wanatakiwa wafanye jitihada za
kupata sare zitakazowatambulisha, filimbi na bunduki mbili ambazo zitatumiwa na
askari wa doria ambao watakuwa wamepata mafunzo ya Mgambo. Alisema katika suala
usajili wa bunduki hizo yeye atakuwa mstari wa mbele kupeleka maombi yao kwa
viongozi wa juu ili waweze kupitisha na hatimaye ziweze kutumika kwenye shughuli
ya ulinzi katika eneo lao.
Kwa
upande mwingine aliwataka mabalozi wa eneo hilo kutafuta askari watakaokuwa
waaminifu ili waweze kufanya kazi zao kwa uadilifu. Mbali na hilo aliwataka
viongozi hao kubuni miradi ya uzalishaji mali ambayo itakuwa moja ya chanzo cha
mapato ya malipo kwa askari hao badala ya kutegemea michango ya wananchi
pekee.
Muroto
alimalizia kwa kuwaomba wananchi wa eneo hilo kushirikiana na Jeshi la polisi
katika kutoa taarifa zinazohusu uhalifu, ambapo alitoa namba za simu za viongozi
wa Jeshi la Polisi mkoani hapa ili ziweze kusaidia kushirikiana kimawasiliano
katika suala hilo. Pia aliahidi kurudi tena katika eneo hilo pamoja na timu yake
kutoa elimu kwa askari watakaoteuliwa kabla hawajaanza kazi rasmi ili waweze
kujua misingi na mbinu mbalimbali za utendaji wa kazi hiyo na hilo ni moja ya
jukumu la Jeshi la Polisi kwa vikundi hivyo.
Awali Mwenyekiti wa
Mtaa wa Kitalu “D” Bw. John kihwele akifungua mkutano huo, alisema kwamba
vikundi vya ulinzi shirikishi vilikuwepo lakini kilichochangia vikundi hivyo
kuyeyuka ni ugumu wa wakazi hao kuchangia vikundi hivyo.
Alisema
pamoja na uwepo wa walinzi karibu kila nyumba lakini uwepo wa vikundi vya ulinzi
shirikishi ni wa umuhimu sana hasa katika kufanya doria za barabara hali ambayo
itasaidia kuimarika kwa ulinzi.
No comments:
Post a Comment