Shirika la Viwango Nchini (TBS) limeitaka Wakala
wa Barabara (Tanroads) kuhakikisha linaweka
matuta yenye uwiano sawa katika barabara zote nchini.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
wa Huduma za Upimaji Ugezi na Vifungashio kutoka TBS,
Agnes Mneney, wakati wa mafunzo kuhusiana na kiwango
cha matuta barabarani.
Alisema TBS wameamua kufikia maamuzi hayo kutokana
na kuwapo kwa tofauti ya ujenzi wa matuta barabarani.
Mneney alisema kuna matuta mengine ni makubwa ukilinganisha
na madhumuni yaliyokusudiwa na pengine huwa ni chanzo cha ajali.
Hata hivyo, alisema madhumuni ya kiwango hicho ni kuisaidia
taasisi na makampuni za ujenzi nchini kuwa na aina moja ya
matuta nchini.
Alisema TBS imeandaa kiwango hiki wakati tayari kulikuwa na
miongozo inayotumiwa na Wakala wa Barabara (Tanroads),
hivyo kiutaratibu ilitakiwa kuwepo na kiwango ndipo miongozo
itolewe.
Mneney alisema shirika limeandaa kiwango kwa kuzingatia maoni
ya wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na miongozo ambayo tayari
inatumika na Tanroads.
Alisema kuwa TBS haitakuwa na kazi ya kusimamia utekelezaji wa
kiwango hicho.
Naye Mhandisi Eliamini Tenga kutoka Tanroad alisema kuwa
awajashirikishwa katika mchakato huo.
Hata hivyo, wamekubali kulitekeleza jambo hilo kuhakikisha
viwango vya matuta vinakuwa katika uwiano mmoja.