MBUNGE wa Mbeya vijijini (CCM) Lackson
Mwanjali ameingia lawamani baada ya wanachi wa Kitongoji cha Italazya kata ya
Ilembo Wilaya ya Mbeya kumtuhumu Mbunge huyo kwa kutoa ahadi hewa ambayo
ameshindwa kuitekeleza.
Mbunge huyo aliwaagiza wananchi hao kujenga shule
ya msingi katika kitongoji chao kutokana na umbali wa shule nyingine
inayosababisha watoto kutembea umbali mrefu kufuata shule.
Mbunge huyo aliwaambia wananchi hao kujenga
majengo ya vyumba vya madarasa hadi kufikia usawa wa mtambaapanya(renta) ambapo
yeye atamalizia kupitia mfuko wa jimbo.
Hata hivyo kufuatia ahadi hiyo hali hiyo imekuwa
kinyume na matarajio ya wananchi hao ambao wamesema tangu atoe agizo hilo
mbunge huyo hajawahi kurudi kijijini hapo wala kutekeleza ahadi hiyo.
Wananchi hao walisema kufuatia hali hiyo
walilazimika kumfuata mara kadhaa mbunge huyo ofisini kwake ili wamkumbushe
kuhusu ahadi yake baada ya wao kukamilisha usawa waliopangiwa na mbunge wao
lakini waliishia kuahidiwa tu.
Aidha wananchi hao walisema Mbunge huyo
amewavunja nguvu baada ya majengo waliojenga kuanza kubomoka hali
iliyosababisha kukatishwa tamaa na utekelezaji wa ahadi hiyo.
"Tumejaribu kumfuata mara kadhaa ofisini
kwake kuhusu kutekeleza ahadi yake hiyo lakini anaendelea kutuahidi hali
inayoonesha kutudanganya tu" alisema Adson Kinga mjumbe wa Serikali ya
Kitongoji.
Alisema juhudi kubwa iliyofanywa na wananchi katika
kujenga majengo hayo ambayo walisema ilikuwa ni ukombozi wa watoto wa
kutotembea umbali mrefu lakini juhudi hizo zimeyeyuka baada ya jengo kuanguka
kutokana na kutoendelezwa.
" Ingekuwa ni kilimo tungekuwa tuko kwenye
mavuno makubwa kutokana na nguvu tuliyoitumia kujenga madarasa hayo lakini
tunasikitishwa na mbunge kutusahau wakati sisi ndiyo tuliomchagua" alisema
Furaha Mwafowela mkazi wa Kitongoji hicho.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo alipotafutwa
kuzungumzia tuhuma hiyo hakupokea simu zake za kiganjani ambazo ziliita mda
mrefu bila kupokelewa.
(Chanzo Mbeya Yetu)
|