Wednesday, November 21, 2012

POLICE


Polisi Waanda Mpango Mkakati Wa Ulinzi Shirikishi

Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto akiongea na wakazi wa Mtaa Kitalu "D" Njiro katika mkutano uliofanyika tarehe 18.11.2012 juu ya uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kitalu "D" Njiro Bw.John Kihwele akihesabu fedha zilizopatikana baada ya Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto (kushoto kwake) kuchangisha fedha hizo kwa njia ya harambee katika mkutano uliowajumuisha, askari Polisi, viongozi wa Mtaa na wakazi wa eneo hilo uliofanyika tarehe 18.11.2012.Jumla ya fedha taslimu Tsh 125,000 zilipatikana papo hapo.
Picha na Mahmoud AhmadArusha
Na: Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha

Wakazi wa Njiro mtaa wa Kitalu “D” wametakiwa kutolifanyia mzaha suala la uanzishaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi kwa madai kuwa wanajitosheleza katika suala hilo. Akiongea na wakazi hao Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto alisema kwamba suala la ulinzi halihitaji ubinafsi wala masihara bali linahitaji ushirikiano wa hali juu.

“Tatizo nililoligundua hapa kila mmoja anaona ameshajitosheleza katika suala la ulinzi kwa kuwa ana mlinzi, kamera na uzio wa umeme, wakati suala hilo linahitaji ushirikiano mkubwa”. Alionya Muroto .

Aliwataka wakazi hao wachukue hatua za haraka juu ya uanzishaji wa vikundi hivyo ili kutotoa mwanya kwa wahalifu kwani udhaifu walionao unaweza kutoa mwanya kwa wahalifu kuvamia eneo hilo.

Alimuagiza Mwenyekiti wa mtaa huo kukaa na wakazi hao ili kupitisha maazimio juu ya uchangiaji wa vikundi hivyo na mara baada ya kukubaliana sheria hiyo itakuwa ni miongoni mwa sheria za serikali ya mitaa hivyo basi yeyote atakayekaidi atachukuliwa hatua.

Aidha aliwataka viongozi wa mtaa huo kuwafahamu watu wote wa eneo hilo hivyo kusaidia kubaini tabia ya kila mmoja na pia kila mtu awe na mawasiliano ya simu na mwezake jambo ambalo litasaidia kupeana taarifa pindi uhalifu unapotokea.

Katika kuhamasisha kufufua vikundi hivyo vya ulinzi shirikishi Mkuu huyo wa Polisi Wilaya alianzisha harambee ya kuchangisha fedha kwa kila mkazi aliyehudhuria mkutano huo hali ambayo ilisaidia kupatikana kwa fedha taslimu Tsh 125,000 papo hapo huku yeye mwenyewe akiwa wa kwanza kutoa mchango wake.

Aliongeza kwa kuwaambia wananchi hao katika kuimarisha vikundi hivyo, wanatakiwa wafanye jitihada za kupata sare zitakazowatambulisha, filimbi na bunduki mbili ambazo zitatumiwa na askari wa doria ambao watakuwa wamepata mafunzo ya Mgambo. Alisema katika suala usajili wa bunduki hizo yeye atakuwa mstari wa mbele kupeleka maombi yao kwa viongozi wa juu ili waweze kupitisha na hatimaye ziweze kutumika kwenye shughuli ya ulinzi katika eneo lao.

Kwa upande mwingine aliwataka mabalozi wa eneo hilo kutafuta askari watakaokuwa waaminifu ili waweze kufanya kazi zao kwa uadilifu. Mbali na hilo aliwataka viongozi hao kubuni miradi ya uzalishaji mali ambayo itakuwa moja ya chanzo cha mapato ya malipo kwa askari hao badala ya kutegemea michango ya wananchi pekee.

Muroto alimalizia kwa kuwaomba wananchi wa eneo hilo kushirikiana na Jeshi la polisi katika kutoa taarifa zinazohusu uhalifu, ambapo alitoa namba za simu za viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa ili ziweze kusaidia kushirikiana kimawasiliano katika suala hilo. Pia aliahidi kurudi tena katika eneo hilo pamoja na timu yake kutoa elimu kwa askari watakaoteuliwa kabla hawajaanza kazi rasmi ili waweze kujua misingi na mbinu mbalimbali za utendaji wa kazi hiyo na hilo ni moja ya jukumu la Jeshi la Polisi kwa vikundi hivyo.

Awali Mwenyekiti wa Mtaa wa Kitalu “D” Bw. John kihwele akifungua mkutano huo, alisema kwamba vikundi vya ulinzi shirikishi vilikuwepo lakini kilichochangia vikundi hivyo kuyeyuka ni ugumu wa wakazi hao kuchangia vikundi hivyo.

Alisema pamoja na uwepo wa walinzi karibu kila nyumba lakini uwepo wa vikundi vya ulinzi shirikishi ni wa umuhimu sana hasa katika kufanya doria za barabara hali ambayo itasaidia kuimarika kwa ulinzi.