14th December 2012
Maoni ya Katuni
Mathalan, wakati wanyama hayawani huweza kutafunana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu sheria zinazowaongoza ni za mwituni, mwenye nguvu mpishe, binadamu hana uhuru huo; wanyama waweza kuzalishana baba na wanawe au mama na wanawe, lakini kwa binadamu ni haramu, uchuro na kinyume cha sheria kutenda hivyo.
Kimsingi binadamu hana hiari katika kufuata kanuni, miiko na sheria ambazo zimekubalika ndani ya mfumo wa jamii. Anayekwenda kinyume cha makubaliano ya pamoja kama walivyosema wanafalsafa wa kale ‘makubaliano ya kijamii’ (social contract) huyo hukutwa na makubwa.
Wakati jamii ya binadamu ikiwa inashi katika misingi ya maelewano na maridhiano hayo, katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio yanaoshiria kwamba bado wapo baadhi ambao wameamua kurejea kwenye mfumo wa maisha ya kihayawani. Hawajijui, wanatenda na kuenenda kama vile hawana uelewa kabisa wa jema na baya.
Juzi mkazi mmoja wilayani Temeke jijini Dar es Salaam amefanya unyama usioelezeka wa kumuua mwanawe kikatili. Kwa mujibu wa habari ambazo ziliandikwa na vyombo vya habari jana, mtuhumiwa ambaye ni mwanamume alimuua mwanawe anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka saba kwa kumcharanga mapanga kichwani na usoni, kisa eti aliingilia ugomvi wa baba yake na mama.
Tukio hili linatokea wakati ndiyo tu taifa hili limetoka kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, kwamba jamii imehamasishwa kutambua kuwa kutenda ukatili dhidi ya wengine siyo jambo jema, ni unyama na kwa kweli ni moja ya vitu vinavyorejesha nyuma juhudi za taifa hili kujikomboa kutoka minyororo ya umasikini.
Tukio la Temeke siyo la kwanza kwa wazazi kuwatendea mambo mabaya na ya kikatili sana watoto wao. Mathalan, kumekuwa na matukio mengine ya kikatili wafanyiwayo watoto na wazazi wao kama kutupa vichanga chooni, kwenye mashimo ya taka; kuwachoma moto; kuwapa vipigo ambavyo havionyeshi kuwa nia ilikuwa ni kuwarekebisha. Kwa ujumla jamii yetu kila uchao inashuhudia mambo ambayo siyo ya kiutu wakitendewa watoto.
Tumesema wanyama hayawani hutenda mambo ya kihayawani kwa kuwa hawajijui, lakini pamoja na uhayawani wa wanyama hawa siyo rahisi mnyama kuruhusu mwanawe kudhuriwa na mnyama mwingine. Kama kuna anayebisha kuhusu hili basi akutane na simba jike mwenye watoto atafahamu tunachosema hapa.
Mara kadhaa sinema za wanyama zilizorekodiwa kwenye mbuga za wanyama zimekuwa zikionyesha jinsi wanyama wa aina mbalimbali wanavyojihami dhidi ya jaribio lolote la kutaka kudhuriwa kwa watoto wao; hawa ni wanyama hayawani, wana uchungu wa ndani sana juu ya watoto wao.
Tunapomtazama mtuhumiwa aliyeua mwanawe kikatili na kinyama kwa kiwango kilichoshuhudiwa huko Temeke juzi, tunajiuliza swali gumu, hivi kizazi cha sasa cha binadamu kimeingiliwa na laana gani kiasi cha kukosa hata utu kwa watoto wake wenywewe?
Huenda jamii sasa imeingiliwa na matatizo makubwa ya kisaikolojia ambayo pengine yanahitaji utafiti wa kisayansi ili kuelewa kwamba vitendo hivi vya kinyama dhidi ya watoto vinachangiwa na nini hasa?
Ubakaji, uchomaji moto, vipigo, kuuawa na aina nyingine za unyama dhidi ya watoto vimekuwa vitendo wanavyofanyiwa watoto na watu ambao walipaswa kuwa wazazi, walezi na walinzi wao. Mambo haya yanatokea na kuripotiwa na vyombo vya habari, lakini jamii inaonekana kuvizoea kiasi kwamba hatua za kitaalamu kubainisa sababu hasa ya mambo haya ni nini, hazichukuliwi na kupewa umuhimu wa kipekee.
Kila tunapotafakari na kujikumbusha vitendo hivi ambavyo vimekuwa vikiripotiwa kila kona ya nchi hii, na hasa tunapoangazia mauaji ya kinyama yaliyofanywa na baba dhidi ya mwanawe, tunatamani sasa jamii iamke na kujiuliza nini cha kufanya kuepusha janga hili linalotaka kuzoeleka nchini.
Ni lazima kila mtu atambue kuwa jamii ina wajibu wa kuwahakikishia watoto usalama wa maisha yao, wakiwa majumbani kwao, wakiwa mitaani (barabarani) na hata wakiwa shuleni. Tujifunze kuwalinda watoto wetu ili kuwaepusha na ukatili unaozidi kuota mizizi ndani ya jamii nchini.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment