Makali ya Dk Mwakyembe
yaanza kukata watuhumiwa
wa ‘unga’
Dar es Salaam. Wafanyakazi wanne wa Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wanaotuhumiwa
kula njama za kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya aina
ya Crystal Methamphetamine, wamesimamishwa kazi.
Mkurugenzi wa JNIA, Moses Malaki, alisema jana, kuwa
utaratibu wa kuwapatia barua umekamilika, kinachofuata ni
utaratibu wa kuunda tume unaotarajia kufanyika wakati
wowote kuanzia jana.
“Tumewapa barua zao rasmi kuwasimamisha kazi leo (jana)
saa 8:00 mchana, kama watakuwa na cha kujitetea, wasubiri
tume itakayoundwa wakati wowote kuanzia sasa,” alisema Malaki.
Alisema tume hiyo itafanya kazi kwa siku 14, ikiwamo kuwahoji
wahusika baada ya hapo itatoa maelekezo serikalini.
Kuhusu watuhumiwa hao kupelekwa polisi, Malaki alisema suala
hilo wanaliachia chombo hicho kutekeleza wajibu wao kisheria.
Hatua hiyo inatokana na agizo la Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe, alilolitoa wiki iliyopita kuagiza wote waliohusika na
njama hizo kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika hatua nyingine, Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na
Dawa za Kulevya nchini, limeomba polisi kumwongezea ulinzi
Dk Mwakyembe kutokana na mapambano yake dhidi ya dawa hizo.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Mwakyembe kutangaza
vita na waingizaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya, wanaotumia
JNIA na kusababisha kuonekana uchochoro wa dawa hizo.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Alhad Mussa Salum, alisema kutokana
na ukubwa wa tatizo hilo nchini, jamii inapaswa kuwa na mikakati
shirikishi ya kuondoa mtandao huo unaotisha.
“Kwa sababu mtandao wa dawa za kulevya unatisha, tunaomba
polisi imwongezee ulinzi Mwakyembe kwa sababu anapambana
na watu hatari na hawatamwacha,” alisema Salum.
Baraza hilo linajumuisha viongozi mbalimbali wa dini zote
wakiwamo masheikh, maaskofu na wachungaji.
No comments:
Post a Comment